POLISI
mkoani Morogoro, inaendelea kuchunguza kilichotokea mpaka mtoto mkoani
hapa, akateswa na mzazi mlezi kwa kuwekwa katika boksi tangu akiwa na
miezi tisa, mpaka alipotimiza miaka minne.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, amesema, baba mzazi wa mtoto
huyo, Rashid Mvungi ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Morogoro alitakiwa kwenda kutoa maelezo kituoni jana lakini hakutokea.
Kamanda
Paul alisema jana kuwa, walimtafuta mzazi huyo kwa simu ili kumkumbusha
umuhimu wa kufika Polisi kutoa maelezo, lakini simu zake zilikuwa
zimezimwa.
Habari
Leo ilifika kwa mwajiri wake katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya
Morogoro, ambako hakuwepo kwa kuwa aliaga kwamba amekwenda katika Kituo
cha Ustawi wa Jamii, alikodai kuwa aliitwa.
Hata
hivyo, mwandishi alipofika katika ofisi hiyo, lilihakikishiwa na Ofisa
Ustawi wa Jamii, Oswin Ngungamtitu, kuwa Mvungi hakuwa amefika katika
eneo hilo, wala hakukuwa na mwito wa yeye kufika katika ofisi hiyo.
Katika
tukio lingine la kutia shaka, Habari leo lilipohojiana na Mvungi
katika nyakati tofauti juzi, alitoa taarifa mbili tofauti, kuhusu sababu
za kumuacha mwanaye kwa mama mkubwa wake, Mariam Said, aliyemuweka
katika boksi kwa zaidi ya miaka mitatu.
Katika
mahojiano ya awali, Mvungi alidai baada ya mzazi mwenzake, Mwasiti
Ramadhan kufariki dunia, alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu
tayari alishakuwa na mke.
Alidai
kwa kuwa alikuwa ameoa, alikubaliana na upande wa pili wa familia ya
marehemu, kuwa mwanaye huyo alelewe na mama yake mkubwa, Mariamu.
Katika
mahijiano na mwandishi mwingine juzi hiyo hiyo, Rashid alidai mwanae
huyo alichukuliwa na Mama yake mkubwa ili kumlea akiwa na umri ndogo na
mara zote alikuwa akipeleka fedha za matumizi.
Alidai
kwa mara ya mwisho alimwona mwanae huyo miezi miwili iliyopita akiwa na
afya ya kuridhisha, wakati taarifa zilizotolewa na Mariam, zilidai kuwa
mtoto huyo hajaogeshwa tangu Julai mwaka jana.
“Kila
nikienda kumwona nyumbani kwao sikubahatika kumwona , nilikuwa
nikiambiwa amelala ama ametoka na watoto wezake...isipo kuwa miezi
miwili iliyopita,” alidai Rashid kauli inayoonesha kuwa mtoto huyo
alikuwa akitoka na wenzake wakati majirani walitoa ushahidi kuwa
hawakuwahi kufahamu uwepo wa mtoto katika nyumba hiyo.
Taarifa
kutoka katika Hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro, zimeeleza kuwa baada
ya uchunguzi wa awali wa afya ya mtoto huyo, alibainika kuwa na
niumonia, ulegevu wa viungo ikiwa ni pamoja na baadhi ya mifupa katika
mwili wake kuvunjika.
Daktari
Mshauri wa watoto, Hores Msaky alipozungumza na Habari leo jana,
alisema walimpokea mtoto huyo juzi akiwa katika hali ya uchafu usio wa
kawaida.
Msaky
alisema waliamua kumfanyia vipimo vya awali pamoja na picha za X ray,
wakagundua kuwa mifupa yake si ya kawaida, inaonekana imevunjika ingawa
hawajajua nini kimemvunja.
“Tunachokifanya hivi sasa ni kujaribu kujua tatizo hilo limetokana na nini,” alisema
daktari huyo .Hata hivyo Msaky alisema kuwa hospitali hiyo haina vifaa
vingi vya kupimia mifupa, hivyo imeshauriwa apelekwe Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi .
Muandishi
wa habari hizi alifanikiwa kuingia wodi aliyolazwa mtoto huyo na
kumkuta akiwa amechangamka, na alipoulizwa anaendeleaje alisema anasikia
maumivu katika sehemu ya kifua .
Mtoto
huyo alikuwa akidhulumiwa haki yake ya utu na kuteswa kwa zaidi ya
miaka mitatu, kwa kufungiwa ndani ya boksi kama mnyama, ili asiamumbukize mama mlezi virusi vinavyosababisha Ukimwi.
Unyama
huo wa kusikitisha, ulikuwa ukifanyika muda wote huo kwa mtoto huyo
Morogoro mjini katika mtaa wa Azimio bila kuripotiwa popote, huku wakazi
na majirani wa nyumba hiyo wakisikia akikohoa na kulia usiku, na baba
yake mzazi akiendelea na maisha kwa kumuogopa mkewe. Wakizungumza na
gazeti hili juzi majirani hao walidai Mariam alihamia katika nyumba hiyo
mwaka 2010, lakini hawakuwahi kumuona akiwa na mtoto.
Hata
hivyo majirani hao walikiri kwamba walikuwa wakisikia mtoto akikohoa na
kulia hasa nyakati za usiku, lakini walikuwa na wasiwasi kuwa huenda
mtuhumiwa alikuwa mshirikina anayefuga watu waliouawa kishirikina au kwa
jina linguine misukule.
Hatimaye
juzi mateso ya mtoto huyo yalipungua, baada ya msamaria mmoja kupata
taarifa sahihi, kwamba ndani ya nyumba hiyo kuna kiumbe asiye na hatia
aliye katika mateso na kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo.
Zongo
akiwa katika kazi za kawaida katika mtaa huo, alipata taarifa kutoka
kwa majirani kuwa kuna mwanamke, Mariamu Said, amemficha mtoto ndani ya
boksi na hamfanyii usafi wala kumtoa nje.
Baada
ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta mwenyeji wake, Mwenyekiti wa
mtaa huo, Tatu Mgagalana na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo
ambapo walimkuta mtuhumiwa, Mariamu na kuanza kumuhoji kuhusu tuhuma
hizo.
Kwa
mujibu wa Zongo, wakati mtuhumiwa akijibu maswali aliyoulizwa huku
akibabaika, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa hali
iliyowapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa Mariamu kwa nguvu,
hatua iliyomuokoa mtoto huyo kutoka katika mateso ya zaidi ya miaka
mitatu.
Ofisa
huyo na mwenyeji wake walimkuta mtoto huyo ametapakaa uchafu uliotokana
na kinyesi na mkojo, kwa kuwa boksi hilo lilikuwa chumba chake cha
kulala, meza yake ya chakula na maji na choo kwa ajili ya haja ndogo na
kubwa.